4 A B C D E F G H I J K L M N O P Q R S T U V W X Y Z
Artists: A - Z > L
Results: 1 to 1 of 9
 • Lady Jaydee

  Country  Tanzania
  Genres pop urban
  Website ladyjaydee.blogspot.com
  FestivalSauti za Busara 2006

  Lady Jaydee
  Lady Jaydee

  Jina la Lady Jaydee ni jina maarufu sana Tanzania hasa katika tasnia ya muziki, ujumbe na uzuri wa nyimbo zake umempa nafasi ya kutambulika ipasavyo ndani na nje ya Afrika Mashariki.

  Jina lake halisi ni Judith Wambura, nyota yake ilianza kung’aa katika umri wa miaka saba alipokuwa anaimba kwaya kanisani mkoani Shinyanga. Alipomaliza elimu yake ya sekondari alijiunga na kituo cha redio cha Clouds Fm kama mtangazaji.

  Aliendelea na kazi yake ya utangazaji ambapo mwanzoni mwa mwaka 2000 alitoa nyimbo yake ijulikanayo kama “Nakupenda” ambayo ilipata nafasi ya kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio vya Tanzania na kisha ikafuatiwa na nyimbo nyingine ya “Mpenzi Wangu”.

  Baadae aliamua kuachana na kazi ya utangazaji na kujikita rasmi katika kazi ya usanii ambapo baadae alifanikiwa kuachia albamu yake ya kwanza iliyopata mashabiki wengi yenye jina “Machozi”. Mwanzo wa mafanikio yake ulikuwa mwaka 2000 ambapo alifanikiwa kuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike ambaye alitoa albamu yake na kisha kufanya ziara mbalimbali za kimuziki katika kipindi cha miaka miwili.

  Mwaka 2003 alifanikiwa kutoa nyimbo zake mbili machachari ambazo ziliwateka mashabiki wa muziki wa Tanzania ambazo ni “Usiusemee Moya” na “Wanaume kama Mabinti”. Mapema baadae aliachia albamu yake ya pili yenye nyimbo 12 ikiwemo ya “Siri Yangu”.

  Nyota ilizidi kung’aa mwaka 2005 alipofanikiwa kutoa albamu yake ya tatu aliyoipa jina la “Moto” ambayo alishirikiana na wasanii mbalimbali wa Afrika kama Samba Mapangala (DRC), TID (TZ) na Titi (Uganda). Alitumia miezi 14 kurekodi nyimbo 18 kati ya hizo ikiwemo ya “Rafiki wa Mashaka” ni hadithi ya kweli ambayo inazungumzia marafiki wanafiki na kuharibu jina la mwanamke, ikafuatiwa na nyimbo yake “Distance” amabyo ilizidi kumpatia umaarufu, aliimba kwa lugha saba tofauti Kiswahili, Kingereza, Kizulu, Lingala, Kifaransa, Kinyarwanda na Kiganda, na kufanikiwa kushikanafasi za juu katika chati za vituo vya radio tofauti kwa zaidi ya mwaka mmoja.

  Mwaka 2006 alizindua rasmi bendi yake aliyoipa jina la Machozi Band ambayo anafanya maonyesho ndani na nje ya Tanzania.

  Mwaka 2011 alifanya onyesho na mwanamuziki kutoka Zimbabwe Oliver Mtukudzi na baadae kutoa nyimbo waliyoipa jina la “Mimi ni Mimi”.

  Takwimu za kampuni ya usambazaji ya GMC inaonyesha kwamba albamu za Lady Jaydee bado zinashikilia rekodi ya kuongoza kwa mauzo.