Press Kiswahili Message

 
From: "Press Kiswahili" <pressnewsletter_sw@PROTECTED>
Subject: Press Kiswahili Message
Date: January 31st 2022

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamasha la Sauti za Busara kuendelea kuteka hisia

Zanzibar, Februari 1: Tamasha la Sauti za Busara litarindima tena Mji Mkongwe, Zanzibar kuanzia Februari 11 hadi 13 huku likiwa na kauli mbiu ya ‘Tunakomaa!’.

Mwaka 2020 na 2021 haikuwa miaka mizuri kwa wasanii, wabunifu na utalii wa kitamaduni kulingana na changamoto ulioletwa Uviko-19.

Sauti za Busara kwa sasa huenda ndiyo tamasha pekee lenye uzoefu wa muziki unaofanyika mubashara wa Kiafrika ambalo hufanyika kila mwaka, linaloonyesha ukomavu, mabadiliko na kusaidia ukuaji wa wasanii.

Muziki wenye ubora wa hali ya juu, huku burudani zikifanyika kwa muda muafaka na huku zikizungukwa na mandhari ya Ngome Kongwe, ni moja ya nembo za kibiashara za tamasha hilo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Paza Sauti: Uwezeshaji Sauti za Wanawake Kusikika’. Tamasha hilo litahusisha orodha ya wasanii wenye vipaji vikubwa kutoka Afrika Mashariki na Kusini, huku kukiwa na kipaumbele kwa wasanii wa kike kutoka Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Zambia na Congo.

Tamasha hili linautangaza muziki wa Tanzania, Zanzibar na Afrika. Kwa miaka 19, limekuwa likikuza tamaduni za Zanzibar na kuukumbatia muziki kutoka katika bara zima la Afrika.

Busara Promotions na mashirika yasiyo ya kiserikali, ndiyo wanaofanikisha tukio zima, wanatambua changamoto wanazokutana nazo wanawake katika kukuza fani vipaji vyao.

Wanazingatia uchaguzi wa wasanii wa kike huku wakiwahamasisha kupanda jukwaani na nyuma  ya pazia. Tamasha pia linatoa fursa kwa wasanii kutumia muziki wao kuimarisha amani, umoja, haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na kuheshimu utofauti wa kitamaduni.

Kwa Watanzania watakaohudhuria tamasha hili watalipa TSh6,000 kwa siku au TSh16,000 kwa siku zote tatu za tamasha.

Sauti za Busara huvutia watu kutoka kila pembe ya dunia ambao wanasaidia kukuza uchumi wa Zanzibar kutokana na wageni wengi kutumia muda wao nchini, wakinunua vinywaji, chakula na bidhaa za asili zinazotengenezwa kwa kutumia mikono na kutalii katika hoteli zilizojengwa katika fukwe za bahari.

Ukiachilia mbali mrengo wa kibiashara na kiutamaduni, tamasha hili ni fursa kwa wasanii, waandaaji wa matamasha, na wadau wa muziki wa Afrika kukutana na kubadilishana uzoefu.

Kila jioni wakati wa tamasha, jukwaa la ‘Movers & Shakers’  hutoa fursa ya wazawa na wataalam kukutana na kubadilishana mawazo.

Viongozi  kutoka katika tasnia ya ubunifu na utamaduni wameshathibitisha kushiriki katika tamasha la mwaka huu.

Sauti za Busara sio tu kivutio cha utalii au burudani pekee, bali ni sehemu ya kujifunza kutokana na uwepo wa hadhira kubwa na mashabiki, likihakikisha misingi kadhaa inazingatiwa kama vile utambulisho, Jamii na ushiriki, ushirikiano na usawa, uhuru wa kujieleza, ubunifu, urithi wa kitamaduni na muunganiko wa tamaduni, na alama inayoachwa ya muda mrefu inayotengeneza kipato, hususan wanawake, Vijana na jamii zilizotengwa.

Mafanikio ya tamasha hili limewezekana kutokana na uungwaji mkono kutoka kwa wahisani, wadhamini na washirika, hususan Ubalozi wa Norway nchini Tanzania ambao ndiyo wamekuwa wakilipa gharama zote za uendeshaji wa tamasha tangu mwaka 2009.

Kwa miaka kadhaa, Umoja wa Ulaya (EU) wamekuwa wakiunga mkono dhamira ya tamasha hili kutangaza kampeni za mazingira, wasanii wa kike, vijana na vipaji chipukizi.

Msaada huo umeiwezesha Busara Promotions kuimarisha uwezo wa kiusimamizi, sera, taratibu na viwango bora katika mipango, usimamizi na utoaji ripoti, mawasiliano na ubadilishanaji uzoefu.

Ilisaidia pia kuwa na ufanisi katika kazi zake na kuandaa tamasha la viwango vya kimataifa kila mwaka.

Kwa kuangalia mustakabali wake na azma ya kuwa tamasha endelevu, matamasha ya Kiafrika yanatakiwa yajitegemee na si kutegemea wahisani wa Ulaya kwa kila kitu.

Pia sekta binafsi ya hapa nchini imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha tamasha hili, shukrani kwa Benki ya CRDB, Zanlink, Emerson Zanzibar, Hotel Maru Maru na washirika wa vyombo vya habari.

Msaada huu haupongezwi tu na waandaaji, Bali hadi Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi katika video ya karibuni ya hotuba yake, aliwashukuru watu wote waliochangia kufanikisha tamasha hilo lenye faida kwa watu wengi.

“Ninaipongeza timu ya Sauti za Busara kutokana na kujitoa kwao na mafanikio yanayoliweka tamasha hilo kuwa hai, Na shukrani za dhati ziende kwa wahisani na wadhamini kwa kufanikisha. Na pia nawapongeza na kuwashakuru wanamuziki ambao wamelifanya tamasha hili kuheshimika na kuvutia watalii wengi kila mwaka,” alisema Rais Mwinyi.

Kulinda mafanikio yaliyopatikana kwa miaka kadhaa na athari zake chanya zitategemea na uwezo wa wadau kutumia vyema jitihada zilizofanywa hadi sasa.

Washirika na wadhamini kutoka katika taasisi binafsi na umma wanahamasishwa kushiriki na kuunga mkono tamasha la msimu ujao, kuhakikisha linaendelea kukua na kufanikiwa.

Tamasha la 19 la Sauti Za Busara linaloanza Februari 11 mpaka 13, 2022 linawezeshwa na Ubalozi wa Norway, Umoja wa Ulaya, CRDB, Zarlink, Emerson Zanzibar na wengineo.

Masharti na taratibu za usalama za Uviko 19 zitaendelea kuzingatiwa. Wataalam wa afya watakuwapo eneo la tukio pale inapohitajika.

Waandaaji wanaendelea kufanya mapitio na kushirikiana na mamlaka za ndani na kuahidi kusimamia afya na usalama kwa wale wote wanaoshiriki au kuhusika na tamasha.

Kwa taarifa zaidi ikiwamo orodha ya wasanii, tembelea: www.busaramusic.org

[Mwisho]

Picha za hi-res zinapatikana: https://www.busaramusic.org/downloads/

 

 

 

  • This mailing list is a public mailing list - anyone may join or leave, at any time.
  • This mailing list is announce-only.

Orodha hii ya kutuma barua imekusudiwa tu kueneza habari zinazohusu Tamasha la Sauti za Busara kwa vituo au vyombo vya habari

Privacy Policy:

Sera faragha ya, Busara Promotions Press : Barua pepe zote katika orodha hii itatumika kwa madhumuni ya kukujuza shughuli zote zinazoendelea Busara Promotions. Hazitatolewa wala kupewa mtu mwingine au taasisi yeyote.