Press Kiswahili Message

 
From: "Press Kiswahili" <pressnewsletter_sw@PROTECTED>
Subject: Press Kiswahili Message
Date: February 8th 2023

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Februari 8, 2023

Kwa nini Sauti za Busara linaendelea kuwa tamasha la kipekee

Unguja. Tamasha la Sauti za Busara la 20 linatarajiwa kuanza Ijumaa, Februari 10, ambapo Stone Town na viunga vyake vitalibeba tamasha hili la burudani ya muziki wa Kiafrika kwa siku tatu mfululizo ndani ya Ngome Kongwe.

Kuna shughuli mbalimbali zinazoendelea katika eneo hilo la kihistoria huku maelfu ya tiketi zikiwa tayari zimeshauzwa kwa wageni wanaotoka katika kila pembe ya dunia.

“Miaka 20 inaweza kuwa ni muda mrefu, lakini kwetu sisi Sauti za Busara na washirika wetu tumeshikamana zaidi katika mambo ya msingi zinazolipa heshima tamasha hili katika mwaka 2023 na wakati huo huo kuhifadhi utambulisho wetu wa kipekee,” anaeleza Yusuf Mahmoud, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara.

Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sana, Tamasha la Sauti za Busara  linajumuisha orodha ya wasanii kutoka kila sehemu ya bara kubwa la Afrika, kutoka Magharibi Kaskazini hadi Kusini, huku wasanii hao wengi wao wakitumbuiza kwa mara ya kwanza visiwani Zanzibar.

“Uchaguzi wa wasanii daima umekuwa moja ya nguzo yetu kwa miaka mingi, wasanii ambao muziki wao ni wa Kiafrika kweli. Huu ukiwa ni mwaka wetu wa 20, tumefanya jitihada za kuleta ladha tofauti za muziki zinazowakilisha utofauti wa Afrika. Hiki ndicho ambacho Sauti za Busara imekuwa ikikikusudia,” alisema mkurugenzi wa tamasha hilo.

Tamasha la mwaka huu linaendeshwa chini ya kaulimbiu ‘Tofauti Zetu, Utajiri wetu.’

"Wasanii watakaotumbuiza mwaka huu ni pamoja na Tiken Jah Fakoly, kutoka Ivory Coast, ambaye anajulikana kama nyota mkubwa wa muziki wa reggae barani Afrika, na BCUC kutoka Soweto, Afrika Kusini, miongoni mwa wasanii wengine bora ambao watalipamba tamasha hilo kwa nyimbo zao za kipekee."

Aliongeza kuwa: Wanamuziki wengi wanaokuja kwenye tamasha hili sio wale unaowasikia kila siku lakini wamekuwa wakifanya makubwa na kuwaacha wahudhuriaji na bumbuwazi.

Kutokana na utofauti huu, tamasha hilo limekuwa kitovu cha utamaduni ambapo jamii kutoka kila sehemu ya dunia hukutana na kubadilishana uzoefu wenye kuacha kumbukumbu zizisofutika.

"Watu wanapokuja katika tamasha la Sauti za Busara, wanaondoka wakiwa na kumbukumbu kutoka kwenye maonyesho na kisiwa hichi ambayo hudumu kwa miaka mingi na wengine wameenda mbali zaidi hadi kutengeneza uhusiano wa kikazi ambao unaendelea katika nyanja zingine za maisha yao," alisema Bw Mahmoud.

Licha ya ukweli kwamba tamasha hilo katika miaka ya hivi karibuni limekabiliwa na changamoto, mafanikio yaliyopatikana yasingewezekana bila ya msaada wa washirika.

“Tumekuwa na washirika kadhaa ambao wamekuwa wakisaidia kulifanya tamasha hili liwe hai hata pale tulipokaribia kukata tamaa kutokana na kukosa fedha. Washirika hao ni pamoja na ofisi za ubalozi, mahoteli, mabenki, wawekezaji na waendelezaji majengo, kampuni za mitandao ya simu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Toleo la mwaka huu pia linashirikisha Movers & Shakers (mitandao kwa wataalamu), Swahili Encounters (ushirikiano wa wanamuziki wa hapa nchini na wageni), matukio ya Busara Plus Fumba Town na maeneo mengine, na Tuzo ya Emerson Zanzibar Music Award, kwa wanamuziki wajao.

Tamasha la 20 la Sauti za Busara, 10 - 12 Februari 2023 limedhaminiwa na, Fumba Town - mradi wa CPS, Ignite Culture, CRDB Bank, Australian High Commission, Ubalozi wa Ufaransa, Ubalozi wa ujerumani, Institut Français, Kendwa Rocks, Mjini FM, ST Bongo Tv, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Adventure247 Marketing Agency, Zanzibar Serena Hotel, Coconut FM, Zanlink, Emerson Zanzibar, 2Tech Security na nyinginezo…

 

Taarifa kwa mhariri : Kwa picha bofya hapa  www.busaramusic.org/downloads

 

  • This mailing list is a public mailing list - anyone may join or leave, at any time.
  • This mailing list is announce-only.

Orodha hii ya kutuma barua imekusudiwa tu kueneza habari zinazohusu Tamasha la Sauti za Busara kwa vituo au vyombo vya habari

Privacy Policy:

Sera faragha ya, Busara Promotions Press : Barua pepe zote katika orodha hii itatumika kwa madhumuni ya kukujuza shughuli zote zinazoendelea Busara Promotions. Hazitatolewa wala kupewa mtu mwingine au taasisi yeyote.